13/08/2026
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma limetoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa vitendo kwa maafisa wa Jeshi la Polisi ngazi ya kata, wilaya na mkoa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo katika shughuli za kila siku.
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, James Vesso, amesema wameona umuhimu wa kutoa elimu hiyo kwa vitendo ili kuwawezesha maafisa hao kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia na kuwafikishia elimu hiyo wenzao pamoja na jamii kwa ujumla.
Vesso amesema matumizi ya majiko ya umeme ni miongoni mwa njia salama na nafuu za kupikia, huku yakitumia muda mfupi ikilinganishwa na baadhi ya njia nyingine za kupikia. Amesema ongezeko la watumiaji wa majiko ya umeme linaendelea kuonekana kutokana na elimu inayotolewa pamoja na ushirikiano wa TANESCO na wadau katika kuwawezesha wananchi kupata majiko hayo.
Ameeleza kuwa TANESCO na wadau wake wamekuwa wakiwezesha wananchi kupata majiko ya umeme kwa mikopo yenye masharti nafuu, ambapo mteja hupewa fursa ya kuchagua utaratibu unaomfaa wa kufanya malipo. Miongoni mwa njia hizo ni malipo kupitia mfumo wa LUKU, ambapo kiasi cha malipo hukatwa kidogo kidogo wakati mteja anaponunua umeme, pamoja na utaratibu mwingine wa kulipa kwa awamu.
Elimu hiyo imetolewa wakati TANESCO Mkoa wa Dodoma ikiendesha kikao kazi maalum na viongozi wa Jeshi la Polisi ngazi ya kata, wilaya na mkoa,Leo 13 August 2026 ambapo pamoja na masuala ya nishati safi, pande hizo zimeweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha ulinzi wa miundombinu ya umeme mkoani Dodoma.
13/08/2026
DODOMA, Agosti 13, 2026
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma limefanya kikao maalum na viongozi wa Jeshi la Polisi ngazi ya kata, wilaya na Mkoa wa Dodoma, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika ulinzi wa miundombinu ya umeme na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika kikao hicho, Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Kuwa Mangara, amesema ushirikishwaji wa vyombo vya ulinzi ni muhimu kutokana na nafasi ya umeme katika maisha ya wananchi na shughuli za kiuchumi, hivyo Jeshi la Polisi linapaswa kuwa sehemu ya juhudi za kuhakikisha miundombinu ya umeme inalindwa.
Amesema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na changamoto za uhujumu na uharibifu wa miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, ikiwemo wizi wa vyuma na bolti, pamoja na uvamizi wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya njia za kusafirisha umeme.
Mangara ameeleza kuwa baadhi ya maeneo hayo yamekuwa yakitumika kwa shughuli za kilimo na uchimbaji wa mchanga na kokoto, hali inayoweza kusababisha mmomonyoko wa udongo na kuhatarisha nguzo pamoja na miundombinu mingine ya umeme. Aidha, ameitaja changamoto ya kuibiwa nyaya zinazotumika kulinda transfoma na kuchomwa kwa nguzo za umeme, hali inayoweza kusababisha kukatika kwa umeme, hasara kwa TANESCO na usumbufu kwa wananchi.
Ametoa wito kwa wananchi kutambua thamani ya miundombinu ya umeme na kuacha vitendo vinavyoweza kuhatarisha upatikanaji wa nishati hiyo, akisisitiza kuwa ulinzi wa miundombinu ya umeme ni jukumu la pamoja kwa TANESCO, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa wa Polisi Jamii Mkoa wa Dodoma, ASP Regina Mtana, amelishukuru TANESCO kwa kutoa elimu hiyo na kuahidi kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na shirika hilo katika kuimarisha ulinzi wa miundombinu ya umeme na kuchukua hatua dhidi ya vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama na upatikanaji wa nishati hiyo.
13/08/2026
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba (Mb.), ameitaka Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma ili wananchi wawe na uelewa mpana kuhusu majukumu ya Wakala na mchango wake katika kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini.
Mhe. Makamba ametoa wito huo alipotembelea banda la PBPA katika maonesho yanayofanyika Viwanja vya Dimbani, Kizimkazi, Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya Tamasha la Kizimkazi 2026.
Amesema ni muhimu wananchi wakaendelea kuelimishwa kuhusu Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja na namna PBPA inavyotekeleza majukumu yake katika kusimamia uagizaji wa bidhaa za mafuta kwa lengo la kuhakikisha nchi inakuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa hiyo muhimu.
Aidha, Mhe. Makamba ameipongeza PBPA kwa utendaji wake katika kutekeleza majukumu yake na kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkaguzi wa Mafuta wa PBPA, Bw. Issa Mwitazy, amemweleza Naibu Waziri kuwa Wakala unaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha nchi inakuwa na kiwango cha kutosha cha mafuta ili kukidhi mahitaji ya soko.
Bw. Mwitazy amesema ushiriki wa PBPA katika Tamasha la Kizimkazi umetoa fursa kwa wananchi na wadau mbalimbali kupata elimu na ufafanuzi kuhusu majukumu ya Wakala pamoja na namna Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja unavyofanya kazi.
Ameongeza kuwa PBPA inaendelea kudumisha ushirikiano mzuri na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) katika masuala yanayohusu sekta ya mafuta.
Tamasha la Kizimkazi 2026, ambalo ni msimu wa tatu, linafanyika kuanzia Agosti 12 hadi 14, 2026, likiwa na lengo la kuibua na kufungua fursa mbalimbali za maendeleo, huku likibeba kaulimbiu “Kizimkazi 2026, Fursa na Shangwe.”
12/08/2026
Mradi wa Tuinuke Pamoja unaotekelezwa na Aga Khan Foundation kwa ufadhili wa Serikali ya Ireland umeendelea kuwafikia vijana katika Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika fursa za kiuchumi na kijamii, pamoja na kuhakikisha makundi yaliyokuwa yakiachwa nyuma yanapata nafasi sawa.
Ofisa wa Mradi huo, Eric Kisiga, amesema mradi huo unatekelezwa katika wilaya za Kondoa, Chamwino, Chemba na Bahi, ukilenga kuimarisha usawa wa kijinsia na kuwafikia vijana pamoja na watu wenye ulemavu ili waweze kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kisiga ameyasema hayo 12 August 2026 jijini Dodoma wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, ambapo amesema vijana wana nafasi kubwa ya kutumia fursa zinazopatikana katika maeneo yao, akiwataka kuanza na kile walicho nacho badala ya kusubiri kuwa na rasilimali nyingi ili kuanza kutekeleza mipango yao.
Amesema maadhimisho hayo yamekuwa pia sehemu ya kuwapa vijana nafasi ya kujadili changamoto na fursa zinazowazunguka, ambapo vijana 25 walishiriki katika mijadala mbalimbali na kuonesha bidhaa wanazozalisha kupitia vikundi vyao, huku wakibadilishana ujuzi na uzoefu kulingana na mazingira wanayoishi.
Kwa mujibu wa Kisiga, kauli mbiu ya maadhimisho hayo, “Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Wote”, inalenga kuhimiza ushirikishwaji wa vijana katika maeneo mbalimbali bila kujali tofauti zao, kiwango cha elimu au mazingira wanayotoka, kwa kuwa wanapaswa kupata haki na fursa sawa katika nyanja za maendeleo, ikiwemo uchumi.
Amesema mawazo na mapendekezo yaliyotolewa na vijana katika maadhimisho hayo yamekabidhiwa kwa Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, ili yatumike katika mchakato wa kutengeneza sera jumuishi ya vijana, huku akiwataka vijana kuacha mipango kwenye karatasi na kuanza kuitafsiri kuwa vitendo kwa kutumia fursa walizonazo.
12/08/2026
Shirika la Equality for Group (EFG), kwa kushirikiana na Aga Khan Foundation kupitia Mradi wa Tuinuke Pamoja, limewawezesha vijana takribani 30 kutoka maeneo mbalimbali nchini kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma leo, Agosti 12, 2026.
Akizungumza kuhusu ushiriki huo, Field Officer wa EFG, Julius Titus, amesema hatua hiyo inalenga kuwaunganisha vijana wanufaika wa mradi na wadau kutoka sekta mbalimbali pamoja na viongozi wa Serikali, ili kuwapa nafasi ya kujenga mahusiano, kupanua mitandao ya mawasiliano na kujifunza fursa zinazoweza kuwasaidia katika maendeleo yao.
Titus amesema kupitia maadhimisho hayo, vijana wanapata fursa ya kubadilishana uzoefu na vijana wengine kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania, kujifunza fursa za kiuchumi, pamoja na kupata maarifa na mbinu mbalimbali za kutafuta masoko ya bidhaa na huduma wanazozalisha.
Amesema ushiriki huo unaendana na kaulimbiu inayosisitiza kuwa “Tuko katika mazingira tofauti lakini fursa sawa kwa vijana,” akieleza kuwa vijana wanapaswa kutambua kuwa Tanzania ni yao na kwamba fursa zilizopo nchini, hususan katika kipindi hiki cha mapinduzi ya kidijitali, zinahitaji ushiriki na ubunifu wao.
Aidha, Titus amewataka vijana kutokata tamaa wala kujibweteka kwa kisingizio cha ukosefu wa ajira, bali kutumia rasilimali na uwezo walionao kuanzisha shughuli zinazoweza kuwainua kiuchumi, huku wakitumia teknolojia na fursa zinazopatikana kulingana na mazingira yao.
Amesema EFG kupitia Mradi wa Tuinuke Pamoja itaendelea kuwawezesha vijana na makundi mbalimbali ya kijamii, wakiwemo watu wenye ulemavu, kwa kuwajengea uwezo na kuwaunganisha na fursa zinazoweza kuchochea usawa wa kijamii na kiuchumi, ili kila mmoja aweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
09/08/2026
Jeshi la Zima Moto na Uokoaji limeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya nishati safi ya kupikia, hususan gesi ya kupikia, pamoja na njia sahihi za kuzuia na kukabiliana na majanga ya moto. Elimu hiyo imetolewa katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu usalama wa moto katika maeneo ya makazi, biashara na shughuli mbalimbali za uzalishaji.
Jeshi hilo limeeleza kuwa limeona umuhimu wa kutoa elimu hiyo katika Maonesho ya Nane Nane kutokana na maonesho hayo kukutanisha maelfu ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini, wakiwemo wakulima, wafanyabiashara, wafugaji, wajasiriamali na wadau wa sekta mbalimbali. Kwa kutumia jukwaa hilo, wananchi wamepata fursa ya kujifunza kwa vitendo namna ya kutumia majiko ya gesi kwa usalama, kutambua vihatarishi vinavyoweza kusababisha moto na kuchukua hatua za tahadhari kabla ya janga kutokea.
Katika utoaji wa elimu hiyo, wananchi wamefundishwa namna sahihi ya kutumia na kuhifadhi mitungi ya gesi, kuhakikisha vifaa vya gesi vinafungwa na kutumika kwa usahihi, pamoja na kuchukua tahadhari wanapobaini dalili za kuvuja kwa gesi. Aidha, wamepewa elimu kuhusu hatua za awali za kuchukua pale moto unapotokea na umuhimu wa kuwa na vifaa vya kuzimia moto katika maeneo yanayohitaji ulinzi huo, huku wakisisitizwa kutotumia njia zisizo salama ambazo zinaweza kuongeza madhara.
Jeshi la Zima Moto na Uokoaji limeendelea kusisitiza kuwa kinga ni hatua muhimu zaidi katika kupunguza madhara yatokanayo na majanga ya moto, hivyo wananchi wanapaswa kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu vyanzo vya moto na namna ya kuvizuia.
07/08/2026
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni, amesema ushiriki wa mamlaka hiyo katika Maonesho ya Nane Nane jijini Dodoma unalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu shughuli za mkondo wa juu wa sekta ya mafuta na gesi pamoja na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la PURA Agosti 7, 2026, Sangweni amesema Tanzania ina maeneo yenye viashiria vya uwepo wa mafuta na gesi asilia, huku tafiti za kijiolojia na tafsiri za data zilizofanyika hadi sasa zikifunika takribani asilimia 30 ya maeneo yanayoaminika kuwa na rasilimali hizo.
Amesema PURA, iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, ina jukumu la kusimamia na kudhibiti shughuli za mkondo wa juu wa petroli, kutoa ushauri kwa Serikali, kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa, kuongeza manufaa ya rasilimali kwa Taifa, pamoja na kusimamia usalama na ulinzi wa mazingira.
Sangweni amesema mamlaka hiyo pia inahakikisha wazawa wanashiriki kikamilifu kupitia ajira, utoaji wa huduma na usambazaji wa bidhaa katika shughuli za mafuta na gesi. Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto ya upatikanaji wa wataalamu wenye ujuzi wa juu na baadhi ya bidhaa zinazohitajika na wawekezaji, hali inayosababisha kutegemea wataalamu na bidhaa kutoka nje ya nchi.
Kutokana na changamoto hiyo, amesema PURA inahamasisha vijana kujenga ujuzi unaohitajika katika sekta ya mafuta na gesi, huku vyuo mbalimbali vikuu vikijumuisha masomo yanayohusiana na sekta hiyo katika mitaala yao. Aidha, Serikali inaendelea kushirikisha taasisi za elimu ya ufundi, ikiwemo VETA, ili kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi wanaoweza kushiriki katika shughuli za sekta hiyo.
Amesema PURA inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ikiwemo kusimamia miradi ya kimkakati katika sekta ya gesi. Miongoni mwa miradi hiyo ni mpango wa kuchakata gesi asilia na kuibadilisha kuwa kimiminika (LNG), unaotarajiwa kujengwa mkoani Lindi kwa lengo la kuiwezesha Tanzania kushiriki zaidi katika soko la kimataifa la gesi.
07/08/2026
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limefanya mkutano maalumu wa ngazi ya juu katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma,07 August 2026 ukiwakutanisha wadau mbalimbali, wawekezaji, watunga sera na wataalamu kujadili namna matumizi ya taarifa za soko yanavyoweza kuimarisha sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ili ziwe na tija zaidi, ziwanufaishe wadau wote na ziwe na ushindani katika masoko ya kimataifa.
Mkutano huo umejikita katika kujadili umuhimu wa taarifa sahihi za soko katika kusaidia maamuzi ya uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za mifugo na uvuvi, kuboresha biashara, pamoja na kufungua fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi. Aidha, umeweka msisitizo katika matumizi ya taarifa hizo ili kuwawezesha wazalishaji na wawekezaji kuendana na mahitaji halisi ya soko.
Akizungumza na Mwandishi Wa habari baada ya kuulizwa umuhimu Wa mjadala huo Joshua Mwakaliule anayejihusisha na Kilimo na ufugaji Wa mbuzi amesema mjadala huo ni muhimu Kwa kuwa matumizi ya taarifa za soko ni nyenzo muhimu katika kujenga mfumo wa chakula na kilimo unaozingatia ushahidi, unaochochea ukuaji wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza ushindani wa bidhaa katika masoko ya kitaifa na Kimataifa.