21/06/2026
SIMULIZI: NAHITAJI NIMFAHAMU
Mtunzi: Ally H.
SEHEMU YA 10
Nilikaa ukingoni mwa kitanda changu kwa masaa kadhaa, macho yangu yakiwa yameganda kwenye kioo cha simu iliyokuwa mkononi mwangu. Ule ujumbe mfupi ulikuwa k**a fumbo zito lililotupa nanga akilini mwangu.
Kwa kawaida, mimi si mtu wa kuamini mambo kirahisi. Maisha yamenichanja chale nyingi za siri, yamenifundisha kuwa kila jambo lina mzizi wake, na kila kivuli unachokiona kina chanzo cha mwanga mahali fulani. Lakini usiku ule, kadri nilivyojaribu kuiliwaza nafsi yangu, ndivyo mapigo ya moyo wangu yalivyozidi kwenda kasi, yakigonga ukuta wa kifua changu kwa fujo.
Nikaufungua tena ule ujumbe, kana kwamba maneno yake yangebadilika.
"Ukifika kwa Mzee Ling’ande… muulize kwanini hakukuambia ukweli wote."
Mwishoni mwa ujumbe huo, kulikuwa na herufi moja tu iliyosimama k**a alama ya kiada.
Z.
Nilizima kioo cha simu. Giza likatanda chumbani, lakini giza kubwa zaidi lilikuwa moyoni mwangu.
Nilinyanyua mkono wangu wa kushoto na kuitazama ile pete. Ilikuwa bado imeng'ang'ania kidoleni mwangu. Lakini haikuwa tena ile pete ya ajabu niliyokusudia kuivua hapo mwanzo. Jiwe lake lililokuwa likimeta sasa lilikuwa limepoteza nuru na kudhoofu.
Hata hivyo, yale maandishi ya siri yaliyokuwa yamechongwa kwa ndani yalikataa kufutika akilini mwangu.
“USIFIKIRI SAFARI IMEISHA.”
Nikainamisha kichwa, nikishika paji langu la uso. K**a kuna kitu kilikuwa kinanitesa usiku ule, haikuwa ile meseji yenyewe. Ilikuwa ni ukweli mchungu kwamba… nilikuwa tayari nimejiaminisha kuwa kila kitu kimefika tamati.
Niliamini dhoruba imetulia. Nimempata Zuwena, mwanamke ambaye angeweza kuyaponya majeraha yangu na kunifanya niamini tena katika upendo. Niliamini pete ilikuwa imetimiza jukumu lake la siri.
Sasa, huu "ukweli wote" unaozungumziwa hapa ulikuwa ni ukweli gani? Je, nilikuwa ninaishi kwenye kivuli cha uongo?
Nilijaribu kuipiga ile namba iliyotuma ujumbe ule. Sauti ya mwanamke wa mtandao ikajibu kwa ubaridi.
"Nambari unayopiga haipatikani kwa sasa..."
Nikajaribu tena na tena. Lakini sikufanikiwa.
Kwa vidole vilivyokuwa vikitetemeka kidogo, nikaandika ujumbe wa maandishi
"Wewe ni nani? Na unataka nini kwangu?"
Nikasubiri.
Dakika ya kwanza ikapita…
Ya pili…
Ya tano…
Kimya kikuu kilitawala. Hakuna jibu.
Usiku ule ulikuwa mrefu na wa mateso. Usingizi ukawa bidhaa adimu kwangu, ukajificha mbali na kope zangu. Kila nilipofumba macho, niliona sura ya Mzee Ling’ande na swali moja lililokuwa likivuma k**a mwangwi milimani. Mzee Ling’ande alikuwa ameficha siri gani kubwa kiasi hicho?
Asubuhi ilipofika, nilijivuta kitandani mapema huku macho yakiwa yamefanya maduara meusi kwa kukosa usingizi. Nilijimwagia maji ya baridi ili kuamsha akili yangu, nikavaa nguo zangu haraka kujiandaa na safari ya kwenda Lindi.
Baada ya kuhakikisha maandalizi yamekamilika. Nilitoka nje, upepo mwanana wa asubuhi ukanipokea. Lakini kabla sijaelekea kituo cha mabasi kuanza safari yangu, moyo wangu ulisikitika na kunivuta upande mwingine. Moyo wangu ulikuwa na kiu ya kumuona Zuwena kabla sijaondoka. Nilihitaji nishati ya tabasamu lake ili nistahimili safari yangu.
Niliingia hospitalini kukiwa na pilikapilika za kawaida za asubuhi. Harufu ya dawa, sauti za chini za wagonjwa na vishindo vya viatu vya madaktari vilitawala korido.
Nilimwona Zuwena kwa mbali. Alikuwa ameketi mapokezi, ameinamisha kichwa chake kwa umakini huku akijaza taarifa kwenye faili kubwa la wagonjwa.
Sikumwita. Nilibaki nimesimama hatua chache kutoka kwake, nikivinjari uzuri wake na utulivu uliokuwa unamzunguka. Alikuwa k**a chemchemi ya maji katikati ya jangwa la mawazo yangu.
Baada ya sekunde kadhaa, kana kwamba alihisi uwepo wa mtu anayemkodolea macho, alinyanyua uso wake. Macho yetu yalipokutana, uso wake uling'aa mara moja na tabasamu pana likachanua midomoni mwake.
"Clever?" alitamka jina langu kwa sauti iliyosikika k**a muziki mtamu masikioni mwangu.
Nikamsogelea na kuegemea kaunta. "Habari ya asubuhi, daktari wangu."
"Nzuri sana. Kumbe bado hujasahau njia ya kuja hospitali?" alitania, huku akicheka kidogo.
Nikacheka pia. "Nilikuwa napita tu hapa karibu." Akakunja midomo yake kwa namna ya kuvutia. "Unasema unapita tu, lakini umesimama hapo ukinikagua kwa dakika kadhaa bila kusema kitu. Hiyo nayo inaitwa kupita?"
Nikaona sina ujanja, nikavuta kiti kilichokuwa karibu na kuketi. Akaendelea kuandika kitu kwenye faili lile kwa sekunde chache, kisha akalifunga na kugeuka mzima mzima kunitazama. Macho yake yakatua kwenye uso wangu, na kwa ghafla, uchangamfu wake ukapungua, ukabadilika na kuwa wa huruma na umakini.
"Leo upo kimya sana, Clever. Kuna nini?"
Nikatikisa kichwa, nikijaribu kuvaa tabasamu la bandia. "Hakuna kitu, ni kawaida yangu tu."
Akacheka kicheko kifupi cha kutokuamini. "Hapana, si kweli."
Nikamwangalia machoni.
Akaniambia maneno yaliyochoma hisia zangu.
"Wewe ukijifanya uko sawa, huwa unasahau kuwa macho yako huwa yanatoa siri yote. Yanasikitika."
Nilishindwa kuhimili macho yale, nikacheka kwa unyonge. "Ah, kweli? Unaanza kunisoma sasa hivi?"
Zuwena alivuta pumzi ndefu, kisha akashusha mabega yake. "Sijui..."
Akatulia kidogo, kisha akasema huku
akinitazama kwa macho yaliyojaa hisia za dhati: "Labda nimeanza kukuzoea sana, Clever."
Nilihisi joto la ghafla likisambaa kifuani mwangu. Tabasamu la kweli lililochochewa na maneno yake likanijia lenyewe. Ili kuficha jinsi nilivyoguswa, nikageuza uso wangu upande wa pili na kumuuliza kwa sauti ya chini.
"Na k**a nikikwambia kwamba nina safari?"
Macho yake yakapanuka kidogo.
"Unaenda wapi?"
"Lindi," nilimjibu kifupi.
Zuwena alibaki kimya. Haikuwa ile hali ya kushangaa ghafla, bali ilikuwa k**a mtu ambaye jina hilo la mahali limeamsha mawazo fulani mazito kichwani mwake.
Baada ya sekunde chache, alitamka taratibu: "Lindi..."
Nikamtazama, nikitaka kusoma nini kiko nyuma ya mtazamo wake. Kuna wakati yalinijia mawazo nitoe simu nimuoneshe ule ujumbe kwenye simu yangu, ile herufi Z ilinifanya niwaze isije kuwa ni yeye Zuwena. Kilichonifanya niwaze hayo ni yale mabadiriko niliyoyaona baada ya kumwambia kuhusu safari yangu ya Lindi, akili yangu ilinikataza nisifanye hivo.
Zuwena alitabasamu tena, lakini safari hii tabasamu lake lilikuwa na chembe ya upweke.
"Sijui kwanini… ila umesema unaenda Lindi, na kwa ghafla nimehisi hii si safari ya kawaida ya kikazi au mapumziko. Kuna kitu kikubwa unachoenda kukifuata."
Nikalazimisha kicheko. "Sasa mbali na utatuzi wa matatizo ya hospitali, umekuwa mtabiri wa safari pia?"
Akacheka kwa sauti ya chini, sauti iliyotulia. "Hapana, mimi si mtabiri."
Akatulia tena, kisha akasema kwa sauti iliyojaa upole uliopenya hadi mifupani mwangu: "Ila… nakuomba usikae sana huko."
Nilimtazama na kumuuliza kwa shauku, "Kwa nini?"
Zuwena aliepuka macho yangu haraka, akajifanya bize kupanga mafaili yaliyokuwa mezani kwake ili kuficha aibu. Kisha akasema kwa sauti ya kunong'ona.
"Kwa sababu..." akatabasamu kwa aibu na kuendelea, "Kuna watu ambao ukishazoea uwepo wao karibu yako… wakiondoka hata kwa siku chache, unaanza kuhisi kuna nafasi kubwa iko wazi. Unaanza kuwamisi"
Nilimkodolea macho, nikizama kabisa kwenye uzuri wa maneno yake.
Aligundua kuwa nimemkazia macho, uso wake ukabadilika rangi kuwa mwekundu kwa aibu, akatazama pembeni haraka sana na kuongeza: "Namaanisha… watu wa nyumbani kwako, mama yako na ndugu zako."
Nikacheka kwa furaha ambayo sikuwa nayo asubuhi yote. "Na wewe je? Utanimisi?"
Akanitazama kwa sekunde mbili, macho yetu yakifanya mazungumzo ya siri ambayo midomo isingeweza kuyasema. Halafu akatabasamu kwa madoido. "Usijisifu sana, Clever. Nenda bwana!"
Tulicheka wote wawili, na lile vazi la huzuni lililokuwa limenitanda likaanza kupungua uzito.
Nilinyanyuka kwenye kiti ili kuondoka. Lakini kabla sijapiga hatua ya tatu kuelekea mlangoni… sauti yake iliniita tena, safari hii ikiwa na uzito wa kipekee. "Clever."
Nikageuka na kumtazama.
Alikuwa amesimama, akinitazama kwa utulivu na umakini mkubwa uliorudisha lile fumbo la usiku uliopita. Kisha akasema.
"Ukirudi… nitafurahi sana kusikia k**a ulifanikiwa kupata kile ulichoenda kukitafuta."
Nilimkodolea macho kwa sekunde kadhaa, nikijaribu kutafakari maana ya kauli yake. Je, alijua kitu kuhusu safari hii? Nilishindwa kupata jibu, nikatikisa kichwa changu tu. "Sawa, Zuwena." Nikageuka na kuondoka.
Nilipotoka nje ya milango ya hospitali, nilihisi upepo ukipita kwenye nywele zangu na nikajikuta natabasamu peke yangu k**a mwehu. Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi ya upweke na maumivu… nilihisi kuna nafsi ya mtu inayonisubiri nirudi kwa hamu. Hiyo ilitosha kunipa nguvu.
Mchana ulipofika, nilikuwa tayari ndani ya basi nikiwa safarini kuelekea Lindi. Ilikuwa ni barabara ile ile niliyopita miezi michache iliyopita. Miti ile ile iliyosimama kando ya barabara, vumbi lile lile.
Mara ya kwanza nilienda Lindi nikiwa kijana aliyevunjika moyo, nikitafuta mwanamke wa kunipenda kwa dhati.
Lakini safari hiyo ya pili. Nilikuwa nimebeba kiu ya kupata ukweli uliokuwa umejificha kwenye giza.
Nilifika jioni sana, sikuweza kwenda moja kwa moja kwa mzee Ling'ande kwani kijiji alipokuwa ni mbali kufika na kuna wakati kunahitajika kupanda usafiri wa boda boda, hivyo ilibidi nisubiri siku iliyofuata.
Mapema siku iliyofuata niliweza kuwasili kwenye eneo alipokuwa akipatika mzee huyo. Nilianza kutembea kwa haraka kuelekea kwenye kijumba kidogo cha udongo cha Mzee Ling’ande.
Eneo lilikuwa tulivu, hakukuwa na watu k**a nilivyokuja mara ya kwanza, Nilipofika kwenye mlango wa nyumba yake… miguu yangu ilikak**aa na kusimama yenyewe, kana kwamba imepigwa shoti ya umeme.
Nyumba ilikuwa imefungwa. Hakukuwa na moshi uliokuwa ukitoka jikoni k**a ilivyokuwa desturi yake. Hakukuwa na harufu ya mitishamba wala dalili yoyote ya kiumbe hai. Kila kitu kilionekana kutelekezwa. Kufuli kubwa la kizamani, lililoshika kutu, lilikuwa limening'inia mlangoni k**a ishara ya kifo cha matumaini yangu.
Nilisimama hapo, nikiwa nimepigwa na bumbuazi, macho yangu yakitamaani kuona hata kivuli cha yule mzee.
Mzee mmoja aliyekuwa anapita njia, akiwa amebeba jembe begani, alisimama na kunitazama kwa huruma.
Sura yangu ya kigeni na mshtuko uliokuwa usoni mwangu ulimfanya anisogelee.
"Kijana, unamtafuta nani mahali hapa?" sauti yake ilikuwa ya kizee na yenye mikwaruzo.
Nikageuka kumtazama, sauti yangu ikitoka kwa tabu. "Namtafuta… Mzee Ling’ande. Mwenye nyumba hii."
Yule mzee alinitazama kwa muda mrefu, macho yake yakibeba ujumbe mzito wa majonzi kabla hata hajayatoa mdomoni mwake. Akavuta pumzi ndefu ya majonzi, kisha akasema kwa sauti ya chini iliyozama masikioni mwangu k**a bomu.
"Kijana wangu… umesikitisha. Umechelewa sana."
Kifua changu kilikaza, nikakunja uso kwa hofu. "Kivipi, mzee wangu?"
Yule mzee alitikisa kichwa chake kwa masikitiko, akatazama ile nyumba iliyofungwa, kisha ak**aliza matumaini yangu yote yaliyosalia.
"Mzee Ling’ande hatunaye tena. Alifariki dunia mwezi mmoja uliopita."
Nilihisi k**a dunia imesimama kuzunguka. Kitu kizito na chenye baridi kali kilipita kifuani mwangu, kikininyima uwezo wa kuvuta pumzi.
Macho yangu yalileta ukungu nikiiangalia ile nyumba iliyobeba siri ya maisha yangu.
Niliuliza tena, kwa sauti ya tetemeko na ya chini kabisa, kana kwamba majibu yangekuwa tofauti.
"Unasema… mwezi mmoja uliopita?"
Usikose Sehemu ya 11...
Karibu kwa maoni na ushauri.......
19/06/2026
19/06/2026
18/06/2026
16/06/2026
15/06/2026