04/06/2026
Je, Jumba la Taifa la Sanaa (National Gallery) ndilo suluhisho la changamoto za wasanii wa Tanzania ?
Kwa miaka mingi, kumekuwa na wito wa kuanzishwa kwa Jumba la Taifa la Sanaa. Bila shaka, taasisi hiyo ni muhimu katika kuhifadhi urithi wa kisanii wa taifa na kutoa nafasi ya maonesho ya kiwango cha juu.
Lakini tunapaswa kujiuliza swali muhimu zaidi:
Je, jumba moja la sanaa litawafikia wasanii wote wa Tanzania?
Wasanii wengi wanaishi na kufanya kazi katika mikoa, wilaya na vijiji mbalimbali. Jumba la Taifa la Sanaa litakuwa sehemu muhimu ya mfumo wa sanaa, lakini haliwezi kuwa suluhisho pekee la changamoto za upatikanaji wa nafasi za kujifunza, kuonesha kazi, kufanya mazoezi na kukuza vipaji.
Tanzania iliwahi kuwa na Vituo vya Maendeleo ya Jamii (DDCs) k**a DDC Mlimani, DDC Magomeni Kondoa, DDC Kariakoo, Keko, na maeneo mengine mengi bila kusahau STEREO( Kinondoni Stereo, Chang'ombe Sterio, Temeke Sterio na zaidi. Vituo hivi vilikuwa sehemu za vijana kujifunza, kuunganishwa na fursa mbalimbali za ubunifu. Leo, vingi vimebadilishwa matumizi na kuacha pengo kubwa katika maendeleo ya sanaa na vipaji.
Labda mjadala wetu usiishie kwenye Jumba la Taifa la Sanaa pekee.
Labda ni wakati wa kuanza kuzungumzia ufufuaji wa vituo vya sanaa na utamaduni katika ngazi za jamii — maeneo yatakayokuwa karibu na wananchi, yatakayohudumia sanaa zote, na yatakayowezesha vijana kujiajiri kupitia vipaji vyao.
Tunahitaji siyo jengo moja la kitaifa pekee, bali mtandao wa vituo vya ubunifu vinavyofikika kwa maelfu ya vijana nchini kote.
Sanaa ni maendeleo. Vipaji ni mtaji. Na jamii ndiyo mahali ambapo vipaji huanza kukua.
Unadhani nini? Je, kipaumbele kiwe Jumba la Taifa la Sanaa au Vituo vya Sanaa vya Jamii?
08/04/2026
26/02/2026